bodi



BODI YA USHAURI YAZINDULIWA TEMEKE HOSPITALI



Dar es Salaam. Bodi ya Ushauri ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Temeke,

ambayo uteuzi wake ulifanywa na Mheshimiwa Ummy Ally Mwalimu, Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto, Septemba 2019, ilizinduliwa rasmi na Mkurugenzi wa Sheria kutoka Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Nd. Luvinga Merick,tarehe 10 Disemba, 2019. Akizindua bodi Luvinga alisema, lengo la kuwa na bodi ni kuweka na kuimarisha misingi ya utawala bora katika kutoa huduma na kwamba bodi ni kiunganishi kati ya hospitali na jamii ambayo inahakikisha kuwa hospitali inatimiza malengo. Uzinduzi wa Bodi hiyo ulihudhuriwa na wajumbe wa Timu ya Uendeshaji wa Huduma za Afya, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa (RRHMT) pamoja viongozi wa Wizara ya Afya.


Bodi iliyozinduliwa ina jumla ya wajumbe 13, ambao uteuzi wao huzingatia sifa na vigezo vilivyowekwa pamoja uwakilishi mbalimbali, hawa ni:- Dkt, Mashombo Mkamba, (Msaafu na Mwakilshi)ambaye ndiye Mwenyekiti wa Bodi, Nd.Ibrahim Zambi (Vyama vya Wafanyakazi), Nd. Said Abdul Kambangwa (Asasi za Jamii (CSO), Nd.Vedasto Mareale Rwiza (Mtaalam wa Fedha), Nd. Julius Nyakazilibe Pius (Vituo vya Afya  - Jamii), Nd.Rose Shao Mlay (Asasi za Kijamii (CSO), Nd. Placidia Grace Barongo (Mwakilishi wa Jamii Watumiaji huduma), Nd. Shani Christoms Mligo (Mwanasheria/wakili), Dkt. Brenda Maria S. D (Hospitali za Asasi Binafsi), Nd. Eunice Muganyizi Bandio (Vyama vya Wafanyakazi), Dkt. Yudas Ndungule (Mganga Mkuu wa Mkoa), na Dkt. Meshack Shimwela (Mkurugenzi wa Hospitali), ambaye pia ndiye Katibu wa Bodi. Kuzinduliwa kwa Bodi ya Ushauri kuliashiria kwanza, kuiingiza rasmi kazini na pili, kuiwezesha kuanza kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria.

Katika siku ya uzinduzi, bodi ilipokea taarifa ya hospitali kuiwezesha kufahamu kazi na majukumu ya taasisi, huduma zinazotolewa, idadi ya wagonjwa wanaohudumiwa kwa siku, hali ya watumishi, hali ya dawa na vifaa tiba pamoja na hali ya fedha na miundombinu. Aidha, bodi ilijulishwa kuwepo kwa mafanikio na changamoto katika hospitali hiyo ikiwa ni pamoja na jitihada mbalimbali zinazofanywa kukabiliana na changamoto.


Vilevile mwelekeo waa taasisi ulibainishwa. Baadhi ya mafanikio yaliyopatikana yalitajwa kuwa ni matumizi ya mfumo wa kielektroniki wa GoTHOMIS katika kukusanya mapato na kufanya malipo ya Serikali kwa kutumia mfumo wa GePG. Mengine ni kufanyika kwa ukarabati wa miundombinu ya hospitali na majengo kwa asilimia 25. Taarifa ilieleza kuwa changamoto kubwa za hospitali ni upungufu wa  watoa  huduma kwa asilimia 38, uchakavu wa gari ya kubebea wagonjwa na uhaba wa maeneo ya kutolea huduma za utakasishaji (CSD), sehemu ya kufulia nguo za hospitali (Laundry), na wodi ya wagonjwa mahututi (ICU), Mkurugenzi wa Hospitali aliongeza kwa kutaja juhudi zilizofanyika kukabiliana na changamoto hizo kuwa ni kuweka vipaumbele kwenye mpango kazi wa hospital (CHOP, 2019/20), upanuzi wa madirisha ya kutolea huduma za dawa na huduma za dharura pamoja na kuboreshwa kwa huduma za kiibingwa.

Taarifa hiyo, ilifuatiwa na kipindi cha mafunzo elekezi ambayo yalilenga kuwaongezea wajumbe wa bodi maarifa na uelewa zaidi wa majukumu yao. Uwezeshaji wa mafunzo ulifanywa na wataam wabobezi kutoka Wizara ya Afya ambao ni Nd. Wilson Jacob Nyamanga, Mkurugenzi Mdaidizi, Masuala ya Utawala na Rasilimali Watu na Luvinga Merick, Mkurugenzi wa Sheria. Aidha, Mlezi wa Hositali ya Temeke kutoka Wizarani, Nd. Romana Sanga naye alihudhuria.


Mafunzo yaliyotolewa yalikuwa chachu na fursa kwa wajumbe kuelimishwa katika nyanja za: Utawala na Rasilimali Watu, Maana na umuhimu wake rasilimali watu katika taasisi. Walielezwa kuwa utawala na rasilimali watu ndio ‘hub’ ya taasisi. Wasisisitiziwa kuwa rasilimali yoyote ni adimu, inahitaji ilindwe na kutunzwa hasusani rasilimali watu. Eneo lingine lilikuwa juu ya wajibu na jukumu la bodi katika kusimamia utawala na rasilimali watu na kwamba, ilitahadharishwa endapo usimamizi utakuwa hafifu matokeo yake ni pamoja na taasisi kukosa usimamizi thabiti wa mipango yake kwa kuwa na uongozi holela, watumishi kufanya watakavyo na kupelekea huduma hafifu. Matokeo mengine ni kuwepo kwa mianya mingi ya rushwa.


Nyanja nyingine ya elimu iliyotolewa ilihusu mfumo wa sheria nchini, unaoanza na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambayo ndiyo sheria mama. Masuala ya Sera ikiwemo Sera ya Taifa ya Afya ya mwaka 2007, Makundi yake yaani Sheria Kuu na Sheria Ndogo yalibainishwa. Wajumbe walielimishwa juu ya Kanuni na jinsi zinavyotungwa na kupitishwa na Bunge pamoja na Miongozo mbalimbali kwa ajili ya utekelezaji wa Sheria.


Wajumbe walijifunza kwamba Sheria, kanuni na taratibu zina umuhimu mkubwa kwani hizo ndizo nyenzo za utekelezaji wa majukumu ya kila siku katika taasisi ikiwemo majukumu ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Temeke.

Aidha, wajumbe walijifunza juu ya Sheria katika Sekta ya Afya, nakuelezwa kuwa zipo zaidi ya 30 ambazo zimewekwa kwenye makundi matano ya:

Sheria za usajili wa wataalam mbalimbali, kila utaalam una usajili wake

Sheria za udhibiti wa magonjwa mbalimbali

Sherai za uanzishwaji wa taasisi chini ya Wizara

Sheria ya Bima ya Taifa ya Afya

Sheria za usajili ya sehemu za utoaji wa huduma


Mchanganuo wa sheria zilizopo katika kila kundi ulitolewa, mfano kundi la kwanza baadhi ya sheria zilizopo ni: Sheria ya Madaktari na Madaktari wa Meno na wataalam wa Afya Shirikishi Na. 11 ya 2007, Sheria ya Wataalam wa Maabara Na.22 ya 2007, Sheria ya Wauguzi na Wakunga Na.1 ya 2010, Sheria ya upeo wa macho kuona Na. 21 ya 2007, Sheria ya Famasi Na. 1 ya 2011, Sheria ya Wataalam wa Afya ya Mazingira Na.20 ya 2007 nk. Mchanganuo wa sheria ulitolewa kwa makundi mengine.


Mwisho wajumbe walifundishwa juu ya wajibu wa bodi na kuelezwa kuwa bodi:

Ina wajibu wa kupata taarifa za hospitali zinazohusiana na utoaji huduma, na hivyo, wataalam waliaswa suala linalotatiza utoaji huduma waishirikishe bodi.

Kushauri na kuidhinisha mpango mkakati wa hospitali na mpango wa uendeshaji wa hospitali

Kufuatilia, kusimamia na kutathmini utekelezaji wa mpango

Kushiriki katika kupokea misaada, zawadi na rasilimali mbalimbali za hospitali

Kupitia na kuishauri Wizara na menejimenti ya hospitali kuhusu makubaliano ya mikataba

Kusimamia ubora wa huduma zinazotolewa katika hospitali ziwe zinazokidhi matakwa ya  wananchi

Kushughulikia malalamiko

Kupokea taarifa za kitaalam, utawala na fedha

Kubuni vyanzo vya mapato.


Pamoja na wajibu, wajumbe walielimishwa kuwa zipo nyenzo kadhaa za kuisaidia bodi kutekeza majukumu yake. Nyenzo hizo ni: Sera ya Afya ya mwaka 2007, Mpango Mkakati wa Nne wa Sekta ya Afya (2016 - 2020), Mpango Mkakati wa Hospitali, Mwongozo wa Uandaaji wa Mpango wa Mwaka wa Hospitali (CHOP), Mpango wa Mwaka wa Hospitali (CHOP), Taarifa za Utekelezaji nk. Iliongezwa kuwa‘’kazi ya ushauri ni ngumu, hivyo, lazima kujua nini bodi inachotakiwa kushauri’’


Wakati wa kufunga mafunzo Mwenyeliti wa Bodi aliwashukuru wawezeshaji wa mafunzo elekezi kwa elimu na maarifa ambayo yamepatikana katika hafla ya kuzinduliwa kwa Bodi ya Ushauri ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Temeke na kusema ‘watajitahidi kufanya yale yote yanayowezekana’’. Mwisho kabisa aliishukuru menejimenti ya hospitali kwa maboresho yanayoendelea kufanyika katika hospitali hiyo.